Dira na madhumuni
Policy Forum ni mtandao wa asasi zisizo za kiserikali. Mtandao huu unaokua kwa kasi, hivi sasa una asasi wanachama zaidi ya hamsini ambazo zote zimesajiliwa hapa Tanzania. Nia na madhumuni ya Policy Forum ni kufanya sera zinufaishe watanzania kwa ujumla, na hasa zaidi watu walio katika hali ya umaskini. Kama mtandao unaoendeshwa na asasi wanachama, Policy Forum inadhamiria kuwezesha jamii kwa ujumla kujihusisha katika michakato ya uundwaji na utekelezaji wa sera huku ikilenga zaidi uondoaji wa umaskini, usawa, na ukuzwaji wa demokrasia nchini. Shughuli za Policy Forum hasa zimelenga katika sehemu tatu: utawala katika serikali za mitaa, matumizi ya fedha za umma, na ukuzaji wa sauti ya umma katika sera na mikakati mbalimbali.
Ikishirikiana na asasi na taasisi zingine, Policy Forum inaendesha shughuli zake kwa kuhamasisha na kutetea sera zilizoboreshwa kwa njia ya uchambuzi madhubuti. Siku za nyuma, Policy Forum imewahi kuhusika katika programu ya Mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUKUTA), tathmini ya matumizi ya pesa za umma, na mikutano ya umma katika uundwaji wa sheria. Vile vile, Policy Forum inashughulika katika kukuza sera za raia na kuwapa wananchi habari na takwimu kupitia redio, machapisho na hii tovuti.